@wepesitv: Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Elizabeth Chacha Mgushi mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa Mtaa wa Ziwa Kata ya Butimba Wilaya ya Nyamagana kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa alitekwa na Watu wasiojulikana waliomtaka kulipa Sh 800000 ili aachiliwe huru. Kwa mujibu wa taarifa za Polisi tukio hilo lilianzia Julai 25 2026 baada ya Mtuhumiwa kuwaacha Watoto wake wanne wenye umri mdogo wakiwa wamelala akiwemo Mtoto wa miaka miwili, bila uangalizi kisha kuondoka kuelekea Mkoani Singida kuonana na mchepuko wake ambapo akiwa njiani alitoa taarifa kwa mume wake akidai ametekwa na Watu wasiojulikana waliokuwa wakidai fedha za kumwachia huru. Aidha, Polisi walianza uchunguzi na ufuatiliaji mara baada ya taarifa hiyo kuripotiwa na kufanikiwa kumtia mbaroni Mtuhumiwa Julai 26 2026 akiwa salama na mwenye afya njema ambapo katika mahojiano ya awali alidai kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na migogoro ya ndoa na kutingwa na majukumu ya familia, huku akieleza kuwa mume wake ambaye husafiri mara kwa mara kwa shughuli za biashara alikuwa hajarejea Nyumbani kwa takribani miezi minne. Jeshi la Polisi limesema chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya mahusiano ya kimapenzi na kwamba Mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa, huku taratibu za kisheria zikiendelea ili afikishwe Mahakamani kujibu tuhuma za kutoa taarifa za uongo.