@defederico99: Video ya Sir Alex Ferguson akiingia Old Trafford kushuhudia mechi ya Manchester United dhidi ya Ipswich imenifanya niwaze vitu vingi sana. Si tu kwenye soka bali pia safari ya maisha kwa ujumla. Huyo mzee anayeingia uwanjani kwa fimbo ya kutembelea huku mguu mmoja ukionekana kutokuwa sawa ni mzee wa miaka 84. Leo anatembea hivi lakini alikuwa kijana mwenye nguvu, mwepesi tena mchezaji kabla ya kuwa kocha. Leo sitaki kuzungumzia rekodi zake kama kocha mwenye makombe mengi zaidi duniani. Sitaki kugusia jinsi alivyoifanya Man United kuwa moja ya timu kubwa duniani. Timu yenye mafanikio makubwa England. Timu yenye mashabiki wengi. Sina mpango wa kuelezea mataji yake 13 ya EPL na jinsi alivyotawala soka la Uingereza. Picha hiyo mjongeo ya Babu Fegi inanifundisha vitu vikubwa viwili tu; mwanzo na mwisho. Hizi ndizo kanuni kuu za maisha. Kuzaliwa na kufa, kulala na kuamka, kuanza kazi na kumaliza, kusaini mkataba na kustaafu, kuanza masomo na kuhitimu, naam kila chenye mwanzo kina mwisho. Kuna watu waliohitimu kidato cha sita juzi tu hapa, wakashangilia sana. Sasa wanaenda kuanza masomo ya chuo kikuu. Wapo wanaotarajia kufanya mahafali ya kuhitimu shahada za awali, shahada za umahiri n.k. Lakini miaka michache iliyopita ilikuwa ni mianzo ya kile kilichofika mwisho sasa. Mwisho huu ndio mwanzo wa fursa zingine za maisha ya kazi. Wapo walioanza mahusiano jana, juzi, mwezi uliopita, mwaka jana na zaidi. Tena walianza kwa mbwembwe na fujo zote za maneno matamu, ahadi kibao, kuchati mpaka saa nane usiku, kupigiana simu za jumla na rejareja, video calls na kila kitu. Si unajua tena penzi jipya. Wapo waliyoyamaliza ndani ya muda mfupi tu baada ya kushindwa kupata suluhu ya tofauti zao. Wapo waliodumu muda mrefu lakini bado mwisho ukafika, wakaachana. Mwanzo wa mechi ni kipenga kimoja. Mwisho wa mechi ni vipenga vitatu. Mwanzo wa mechi kila timu ina morali ya kushinda lakini mwisho wa mechi wengine hulia na wengine hushangilia. Mwanzo wa maisha mtoto analia. Mwisho wa maisha marehemu analiliwa. Katika kila kitu tunachofanya, haijalishi mwanzo ulikuwa mtamu au mchungu kiasi gani; cha msingi tuwe na mwisho mzuri. Mwisho mzuri kwenye biashara, safari, kazi, ndoa na zaidi ya yote mwisho mwema wa maisha yetu hapa duniani.
Federico99
Region: TZ
Monday 31 August 2026 06:24:47 GMT
Music
Download
Comments
There are no more comments for this video.
To see more videos from user @defederico99, please go to the Tikwm
homepage.